Aliyekuwa Waziri na mbunge wa Chepalungu John Koech ameaga dunia akipokea matibabu katika hospitali moja Jijini Nairobi.
Rais William Ruto, ameliongoza taifa kumwomboleza marehemu Koech, akimtaja kuwa kiongozi aliyejitolea kuwahudumia Wakenya.
“Mheshimiwa John Koech alikuwa mwemye bidii aliyewahudumia wakazi wa Chepalungu kwa kujitolea. Alikuwa na mwelekeo mwema na aliyetekeleza maendeleo,” alisema Rais Ruto katika ujumbe wake wa rambirambi.
Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, kwa upande wake, alimtaja Koech kuwa shujaa wa usawa na aliyesababisha kunawiri kwa elimu hasa katika zilizokuwa wilaya za Kericho na Bomet, ambako aliwafungulia vijana wengi milango ya elimu.
“Nilipata fursa ya kuhudumu pamoja na Mheshimiwa Koech wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki. Nilishuhudia mtu aliyekuwa na msimamo thabiti na aliyekumbatia maendeleo,” alidokeza Wetang’ula.
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen vile vile alituma risala za rambirambi, akimtaja Koech kuwa kiongozi shupavu.
“Nimehuzunishwa na kifo chake. Natuma rambirambi kwa familia, marafiki na wakazi wa Chepalungu, ambao aliwawakilisha bungeni kwa muda mrefu,’ aliongeza Murkomen.