Maafisa wa asasi mbali mbali za usalama, wameanzisha uchunguzi kuhusu mlipuko wa kifaa cha kujitengenezea (IED), kilichotokea Jumatatu asubuhi katika eneo la Shafshafey, kaunti ya Mandera ambapo mtu mmoja alijeruhiwa.
Kulingana na idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), maafisa hao waligundua kuwa kilipuzi hicho kiliharibu paa la hoteli na kusababisha nyufa kwenye ukuta.
DCI ilisema wakati wa tukio hilo, wateja wanne walikuwa katika hoteli hiyo,watatu walinusurika huku mmoja akipata majeraha na kupelekwa katika hospitali ya rufaa ya Mandera ambako anaendelea kupokea matibabu.
Aidha uchunguzi wa awali umebainisha kuwa, wawili kati ya walionusurika,wanashukiwa kupanga shambulizi hilo. Maafisa wa polisi wamewatia nguvuni, uchunguzi ukiendelea.
Wakati huo huo, maafisa wa polisi wanamtafuta mwendasha pikipiki aliyewasafirisha wawili hao hadi katika hoteli hiyo, muda mfupi kabla ya mlipuko huo.