Kenya inaweka mipango kabambe kwa lengo la kuhakikisha inaibuka kuwa kituo kinara katika matumizi ya akili mnemba (AI) barani Afrika.
Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi anasema kwa kuwa kituo kinara cha AI barani humo, Kenya itakuwa mfano wa kuigwa katika uvumbuzi, kuchochea maendeleo endelevu, ukuaji uchumi na jamii jumuishi.
Mudavadi anasema Kenya inalenga kuongoza katika utafiti wa AI na matumizi ya teknolojia hiyo kwa kuzingatia uwezekano wa mabadiliko makubwa yatakayoletwa na AI katika siku zijazo.
“Nchini Kenya, kuna mazungumzo nyeti yanayofanyika na shabaha yetu ni kutekeleza mkakati unatoa mpangokazi madhubuti wa kuongoza Kenya katika kutumia nguvu ya mabadiliko ya AI, kuhakikisha matumizi yake yanafaidi sekta zote za jamii wakati tukizingatia kanuni za kimaadili na ambazo ni jumuishi,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.
“Kama bara, tunahitaji kutojiruhusu kuongozwa na uoga. Uoga haupaswi kutuondoa mjini kuhusiana na hii ajenda ya akili mnemba.”
Mkuu huyo wa Mawaziri aliyasema hayo alipoiwakilisha Kenya katika Kongamano la AI Duniani 2025 lililomalizika hivi mjini Kigali, Rwanda.
Aliongeza kuwa Kenya pia inatazamia kuhakikisha mfumoikolojia wa AI humu nchini ni salama.