Ugonjwa wa surua wasababisha vifo vya watoto wawili Texas

Watoto hao hawakuwa wamechanjwa dhidi ya ugonjwa huo.

Marion Bosire
2 Min Read

Watoto wawili wamefariki kufikia sasa kutokana na ugonjwa wa surua au Measles ambao unaendelea kusambaa katika eneo la magharibi la Texas nchini marekani.

Mtoto wa kwanza wa umri wa miaka 6 ambaye hakuwa amechanjwa dhidi ya ugonjwa huo alifariki mwezi Februari huku mwanaume ambaye pia hakuwa amechanjwa akifariki katika eneo la New Mexico mwezi Machi mwaka huu.

Kifo cha hivi punde zaidi ni cha mtoto wa miaka minane ambaye hakuwa amechanjwa na kilitokea Alhamisi. Vipimo vilionyesha kwamba hakuwa na maradhi mengine ila surua tu.

Naibu Rais wa mfumo wa afya wa UMC huko Texas Aaron Davis alithibitisha kifo hicho pamoja na mazingira yake.

Waziri wa Afya nchini Marekani Robert F Kennedy Jr ambaye tayari amelaumiwa kwa jinsi anavyosimamia mlipuko wa ugonjwa huo anatarajiwa kuzuru jimbo la texas wiki hii.

Serikali ya jimbo hilo imeripoti visa 480 vya ugonjwa wa surua mwaka huu na unaonekana kuenea hadi majimbo jirani.

Davis katika taarifa alisisitiza umuhimu wa chanjo akielezea kwamba ugonjwa huo unaambukizwa haraka na madhara yake ni makubwa mwilini hasa kwa wale ambao hawajapokea chanjo.

Mwaka huu pekee, Marekani kwa jumla imeripoti visa 600 vya ugonjwa wa surua na vingi vilitokana na mlipuko wa mashariki ya Texas.

Visa vya ziada ni katika majimbo ya New Mexico, Oklahoma na Kansas na la kushangaza ni kwamba waathiriwa wote hawakuwa wamepokea chanjo.

Virusi vya surua hudhihirisha dalili kama joto jingi mwilini, vipele vya rangi nyekundu, kikohozi na nyingine. Ugonjwa huo unahusishwa pia na nimonia, ubongo kufura na kifo.

Mwaka 2000 Marekani ilitangaza kwamba imetokomeza kabisa ugonjwa wa surua lakini visa vimeripotiwa tangu wakati huo huku wengi wakikosa kupokea chanjo.

Website |  + posts
Share This Article