Simba wa Bongo wanyongwa Misri

Simba, waliishiwa na maarifa na kumenywa mabao mawili bila jibu na Al Masry ya Misri

Dismas Otuke
1 Min Read

Miamba wa soka wa Tanzania bara, klabu ya Simba, waliishiwa na maarifa na kumenywa mabao mawili bila jibu na Al Masry ya Misri, kwenye mkondo wa kwanza wa robo fainali kuwania Kombe la Shirikisho barani Afrika jana Jumatano jioni.

Mchuano huo uliosakatwa mbele ya mashabiki lukuki wapatao 86,000 ugani Borl El Arab, mjini Alexandria, ulishuhudia wageni Simba, wakifungwa bao moja katika kila kipindi, la kwanza kunako dakika ya 16 kupitia kwa Abderrahim Deghmoum, na la pili kupitia kwa John Ebuka katika dakika ya 89.

Simba wanaolenga kufuzu kwa nusu fainali ya kombe hilo kwa mara ya kwanza, wanakabiliwa na shinikizo la kubadili matokeo hayo wakihitaji ushindi wa mabao 3-0, watakapowaalika Waarabu hao nyumbani jijini Dar es Salaam, tarehe 9 mwezi huu.

Katika matokeo mengine ya mkumbo wa kwanza wa kwota fainali, mabingwa watetezi Zamalek kutoka Misri waliambulia sare kappa dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, Constantine na USM Alger za Algeria zikatoshana nguvu kwa kutoka sare ya bao 1-1, huku RS Berkane kutoka Morocco ikipata ushindi wa goli moja bila jibu ugenini kwa Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Website |  + posts
Share This Article