Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali yake haitamvumilia mtu yeyote ambaye anachochea chuki na uhasama, jambo alilosema linahatarisha umoja na amani ya nchi.
Akizungumza Jumatatu katika Baraza la Eid El Fitr ambalo liliandaliwa Jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi wa kidini, Rais Samia alitoa wito wa kuheshimiwa kwa sehemu za kuabudu akisema hazipaswi kutumiwa kama majukwa ya kuendeleza siasa na kuvuruga amani ya nchi.
“Niwaombe katika madhehebu na makundi yenu mbalimbali, muweze kuwadhibiti wale wachache miongoni mwenu walio na mwelekeo wa kuhubiri na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya serikali yao,” alisema Rais Samia.
Rais huyo alisema Tanzania inafahamika ulimwenguni kote kuwa na amani na utulivu tangu ilipopata uhuru mwaka 1961.
Huku taifa hilo likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu badaye mwaka huu, Rais Samia aliwata viongozi hao wa dini kuhakikisha amani inadumishwa, huku akiwasifu kwa jinsi wanavyojiuepusha na mitafaruku ya kisiasa.
“Mwaka huu tunakabiliwa na Uchaguzi Mkuu, hivyo nawasihi sana viongozi wetu wa kidini tushikilie msimamo wetu wa imani,udhibiti wa nafsi zetu na wajibu wetu katika kuitunza na kuikuza amani yetu nchini,” alisema Samia.
Alizitaka sehemu za ibada kutumika kuleta amani na mshikamano nchini humo.