Kiungo wa zamani Harambee Stars Victor Wanyama amesaini mkataba na klabu Dunfermline Athletic FC, inayoshoriki ligi ya daraja ya pili nchini Scotland hadi mwishoni mwa msimu.
Wanyama aliye na umri wa miaka 33, amekuwa na amali nzuri ya soka akizichezea timu za Celtic, Southampton, Tottenham Hotspur na CF Montreal ya Canada.
Upande wa timu ya taifa Harambee Stars,Wanyama alisakata mechi 64 akiwa nahodha wa kwenye fainali za kombe la mataifa ya Afrika AFCON mwaka 2019, kabla ya kustaafu soka ya kimataifa mwaka 2021.
Alijiunga na klabu ya Southampton msimu wa mwaka 2012 kwa pauni milioni 12.5, akiandikisha historia kuwa Mkenya wa kwanza kupiga soka ya kulipwa katika Ligi kuu Uingereza .
Baadaye alijiunga na Tottenham Hotspur alipokutana na meneja wake wa zamani Mauricio Pochettino na alikuwa katika kikosi cha Spurs kilichoshiriki fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019.
Wanyama aligura klabu ya Montreal ya Ligi kuu nchini Canada Januari mwaka huu, baada ya kukamilika kwa kandarasi yake.