Mahakama kuu yadumisha uamuzi wa Seneti wa kumsimamisha kwa muda Seneta Orwoba

Mahakama ilipata kwamba mamlaka za bunge la seneti hazikukiuka haki za Seneta Orwoba kwa kumsimamisha kuhudhuria vikao vya bunge.

Marion Bosire
2 Min Read

Mahakama huu imedumisha uamuzi wa bunge la Seneti wa kumsimamisha kwa muda Seneta mteule Gloria Orwoba kwa kutupilia mbali ombi la kuzuia kusimamishwa kwake.

Orwoba aliwasilisha kesi katika mahakama ya Machakos akidai kunyanyaswa na washtakiwa wa pili na wa tano katika kesi yake ambao ni karani wa seneti na bunge la Seneti mtawalia mwaka 2023.

Alidai kunyimwa fursa za kusafiri nje ya nchi huku karani wa bunge la seneti akiwapa maseneta fulani fursa hizo.

Karani wa bunge alimwalika Orwoba kwa kikao cha kuchunguza madai yake Agosti 7,2023 cha kamati ya bunge la Seneti kuhusu Mamlaka na mapendeleo.

Orwoba alisema kamati hiyo ilikosa kumpa stakabadhi alizokuwa ameitisha na kuendelea na kikao hicho hata bila uwepo wake.

Kamati hiyo iliwasilisha kwa seneti mapendekezo ya suala hilo ili yapitishwe hatua iliyotekelezwa bila uwepo wake kwani alikuwa nje ya nchi.

Kulingana na stakabadhi za mahakama, Orwoba alidai kwamba hatua zilizochukuliwa zililenga kumnyima fursa ya kujieleza na kujibu inavyohitajika katika kikao chenye usawa.

Alisema pia kwamba alisimamishwa kutoka kuhudhuria vikao vya bunge la Seneti kwa muda uliokuwa umesalia wa awamu ya pili akisema ni kinyume cha haki na ukiukaji wa sheria.

Orwoba alikuwa anatafuta usaidizi wa mahakama kutokana na woga kwamba angepoteza wadhifa wake kama Seneta mteule kwa kukosa kuhudhuria vikao muhimu na kuharibu sifa zake.

Washtakiwa walijitetea wakisema kwamba Orwoba alisimamishwa kutoka kuhudhuria vikao kwa kukiuka kanuni za bunge.

Seneta huyo anadaiwa kuchapisha kwenye kundi la Whatsapp la seneti madai ambayo yaligusa shughuli za bunge hilo. Anaripotiwa pia kuondoka kwenye kikao cha kujadili mienendo yake akidai kwamba kilikuwa na upendeleo.

Jaji Lawrence Mugambi ameamua leo kwamba kutokuwepo kwa Orwoba kwenye vikao hivyo muhimu kwa kupenda kunatoa fursa kwa seneti kumchukulia hatua zinazofaa.

Alitupilia mbali ombi la Orwoba bila kumpa yeyote mzigo wa gharama ya kesi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *