Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amefanya mkutano na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Hisayuki Fujii.
Mkutano huo, uliohudhuriwa na ujumbe kutoka jumuiya ya biashara ya Japani, uliangazia maslahi ya pande mbili na ushirikiano wa kimkakati.
Mazungumzo kati yao yaliangazia Kongamano lijalo la Biashara na Uwekezaji kati ya Kenya na Japani litakalofanyika jijini Nairobi. Walizungumzia fursa zilizopo za kuboresha ushirikiano katika nyanja muhimu kama vile miundombinu, elimu, kilimo, mabadiliko ya tabia nchi na ulinzi.
Akitambua mchango mkubwa wa Japani kwa maendeleo nchini Kenya kupitia msaada rasmi wa maendeleo na uwekezaji katika nyanja muhimu, Mudavadi alisisitiza dhamira ya Kenya kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na Japani uliojikita kwa uhusiano wa kidiplomasia uliodumu miaka 61.
Mudavadi alimhakikisha Fujii juu ya ushiriki wa Kenya katika matukio ya dunia ikiwa ni pamoja na Kongamano la Kimataifa la Tokyo juu ya Maendeleo ya Afrika, TICAD 9, litakaloandaliwa mjini Yokohama nchini Japani mwezi Agosti mwaka huu.