Wakazi wa eneo la Gitambaya katika eneo bunge la Ruiru kaunti ya Kiambu, walibomoa ua uliokuwa umezungushiwa ardhi ya umma ambayo wanasema inalengwa na watu fulani wenye nia mbaya.
Kipande hicho cha ardhi kinaripotiwa kutengwa na serikali ya kaunti ya Kiambu kwa ujenzi wa vituo mbali mbali vya huduma kwa jamii ikiwa ni pamoja na kituo cha teknolojia ya mawasiliano, ukumbi na shule ya chekechea.
Miradi hiyo inafaa kutekelezwa na mpango wa maeneo ya makazi duni ya Kenya kwa ufadhili wa benki ya dunia.
Wakazi hao waliokuwa na ghadhabu wakiongozwa na mwakilishi wadi wa eneo hilo Kimani wa Nduta walilaumu makundi ya walaghai yanayoshirikiana na watu walio na ushawishi mkubwa kwa kupanga kunyakua ardhi hiyo, wakiapa kupinga hatua hiyo.
Ardhi hiyo ambayo iko katika eneo la makazi la Fort Jesus, mkabala na barabara ya Eastern Bypass, ilikuwa imezungushiwa ua wa mabati ambayo wakazi hao waliondoa na kuitaka serikali ya kaunti kuchukua hatua ya kuanzisha miradi iliyokusudiwa.
Kimani alisema ana stakabadhi za kudhibitisha kwamba ardhi hiyo ni mali ya umma, ambayo iligawanywa mwaka 2001 kutoka kwa kampuni ya ufugaji ya eneo bunge la Githunguri na kutengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya umma.
Wakazi walisema eneo hilo lenye wakazi wengi halina vituo muhimu kama shule ya chekechea na kuomba Gavana Kimani Wamatangi kuharakisha kurejesha ardhi hiyo.