Murkomen afika Nyayo House kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa Waziri wa Usalama wa Taifa

Waziri huyo alifahamishwa kuhusu masuala yaliyopatiwa kipaumbele, ufanisi, mipango na changamoto za idara ya uhamiaji na huduma kwa wananchi.

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kipchumba Murkomen leo aliandaa mkutano wa kwanza katika jumba la Nyayo na wakuu wa taasisi mbalimbali zilizo katika idara ya uhamiaji na huduma kwa wananchi wakiongozwa ka katibu Julius Bitok.

Waziri alifahamishwa kuhusu masuala yaliyopatiwa kipaumbele, ufanisi, mipango na changamoto za idara hiyo.

Akizungumza na wanahabari baada ya kuzuru kaunta mbalimbali za huduma katika jengo hilo, Waziri alisema ameridhika na hatua zilizopigwa na idara hiyo katika kuboresha utoaji huduma katika muda wa miaka miwili iliyopita.

Murkomen alishukuru mtangulizi wake Naibu Rais Kithure Kindiki na wafanyakazi wa idara hiyo kwa kuimarisha utoaji huduma hasa utoaji wa pasipoti za usafiri.

Kulingana naye, sasa hati hiyo muhimu inachukua siku saba pekee kutayarisha kutoka muda wa siku 30 uliokuwa ukitumika miaka miwili iliyopita.

Waziri alipongeza pia hatua ya kuweka katika mfumo wa dijitali huduma za serikali hususan kwenye tovuti ya e-Citizen, akisema huduma zilizoko zimepita elfu 5 zilizolengwa mwanzoni.

Alisema kufikia Disemba 2024, huduma za serikali 21,589 zilikuwa zimewekwa kwenye mfumo wa dijitali.

Murkomen aliahidi kushughulika kutatua masuala kama mafunzo, miundombinu, ugatuzi, wafanyakazi na ufadhili wa kuimarisha huduma hata zaidi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *