Serikali ya kaunti ya Nairobi imewaagiza wamiliki magari ya uchukuzi wa umma, kuhakikisha magari yao yanaondoka katika vituo vya kubeba abiria shughuli za usafi zinapoanza katikati ya jiji la Nairobi.
Kupitia kwa ilani iliyoandikiwa chama cha wamiliki wa matatu Jijini Nairobi, serikali hiyo ilisema baadhi ya matatu huwazuia wafanyakazi wa kaunti ya Nairobi kutekeleza shughuli za usafi saa za usiku.
“Magari yote yanapaswa kuondolewa katika vituo vya kubeba abiria shughuli za usafi zinapoanza kutekelezwa majira ya usiku,” ilisema ilani hiyo.
Wakati huo huo, wamiliki hao wa magari ya uchukuzi wameagizwa kuhakikisha matatu zao zinazingatia usafi wa hali ya juu katika juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira.
Ilani hiyo pia iliwataka wamiliki hao wa matatu kupunguza muziki wa sauti ya juu na kupiga honi kiholela.
Magari ya uchukuzi ambayo yameegeshwa katikati ya jiji la Nairobi pia yanapaswa kuondolewa mara moja, ili kutoa fursa kwa shughuli hizo za usafi kutekelezwa.
Serikali ya kaunti ya Nairobi ilianzisha shughuli za kusafisha katikati ya jiji la Nairobi nyakati za usiku kwa lengo la kutunza na kuhifadhi mazingira ya jiji hilo.