Rais William Ruto ameondoka nchini leo jioni kuelekea mjini Abu Dhabi katika Umoja wa Milki za Kiarabu, UAE, kuhudhuria kongamano la Marais kuhusu maendeleo endelevu.
Ruto anatarajiwa kuhutubia kikao hicho cha kuadhimisha wiki ya maendeleo endelevu mjini Abu Dhabi kuhusu hatua zilizopigwa na Kenya kwa matumizi ya nishati safi.
Akiwa Abu Dhabi, Rais Ruto anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi kadhaa akiwemo Rais wa UAE, Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan na Waziri Mkuu wa Malasyia, Anwar Ibrahim kuhusu ushirikiano baina ya Kenya na mataifa hayo katika sekta za teknolojia, uwekezaji, nishati na biashara.
Sekta hizo ni nguzo kuu za mpango wa serikali ya Kenya Kwanza wa kutekeleza mabadiliko ya kiuchuni kuanzia chini hadi juu, BETA.
Aidha akiwa Abu Dhabi, Ruto anatarajiwa kusaini mkataba wa ushirikiano baina ya Kenya na UAE kuhusu kusisimua biashara na uchumi.