Kenya yakataa kung’atwa na Nge wa Gambia

Dismas Otuke
2 Min Read

Harambee Stars ya Kenya ilitoka nyuma mara mbili na kulazimisha sare ya mabao matatu  dhidi ya The Scorpion ya Gambia,  katika mchuano wa kufuzu Kombe la Dunia jana usiku.

Mechi hiyo ya mzunguko wa tano kundini F, iliyosakatwa kiwarani Allasane Quatarra nchini Ivory Coast, ilishuhudia kipindi cha kwanza kikiishia sare tasa licha ya wenyeji kukosa kufunga penati.

Penati ya Musa Barrow iliyokuwa imesababishwa na makosa ya kipa Ian Otieno, ilipanguliwa katika dakika ya 30 na kipa.

Kipindi cha pili Gambia walikuja kwa matao ya juu na kuchukua uongozi kunako dakika ya 50 kupitia kwa Musa Barrow, kabla ya Yakuba Minteh kutanua uongozi huo dakika 11 baadaye.

Nahodha Michael Olunga alikomboa bao moja katika dakika ya 69, kabla ya nguvu mpya Mohammed Bejaber, kusawazisha kunako dakika ya 75.

Musa Barrow aliwarejesha wenyeji uongozini katika dakika ya 84, lakini nguvu mpya William Wilson,  akakomboa kwa Harambee Stars katika dakika ya 96.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa kocha Benni McCarthy,  tangu atwae ukufunzi wa Kenya.

Matokeo hayo yanaiacha Kenya katika nafasi ya nne kwa pointi 6, huku wakijiandaa kuwaalika Gabon Jumapili hii katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.

Ivory Coast watacheza ugenini leo dhidi ya Burundi, ambapo Kenya watafungiwa nje ya kwenda Kombe la Dunia mwaka ujao endapo Ivory Coast, watapata ushindi dhidi ya wenyeji.

 

Website |  + posts
Share This Article