Kampuni ya saruji ya Mombasa yarejelea mipango ya kusaidia jamii

Kampuni hiyo ya Mombasa Cement ilikarabati madarasa yote na kujenga mapya, ikaweka taa, kuchimba kisima cha maji na kujenga vyoo 16 katika shule ya Mkwajuni.

Marion Bosire
3 Min Read

Wakazi wa kaunti za Mombasa na Kilifi wana sababu ya kufurahi baada ya kampuni ya saruji ya Mombasa kurejelea mipango ya kusaidia jamii katika eneo hilo.

Akizungumza katika shule ya msingi ya mkwajuni, huko Kilifi Kaskazini, ambapo alikabidhi madarasa mapya manne, vyoo 16 na kompyuta afisa wa mipango ya kijamii wa kampuni hiyo, Mohamed Amir alisema hakuna mipango yoyote itakayofutwa.

Kulingana naye, mipango hiyo ya kusaidia jamii inajumuisha ya utoaji chakula, maji, udhamini kwa wanafunzi wenye vipaji na wenye mahitaji na ujenzi na ukarabati wa taasisi za umma na binafsi.

Malalamiko yalisheheni kaunti hizo mbili baada ya mipango hiyo kusitishwa kwa muda, hatua ambayo ilisababisha mshtuko kwani ilinufaisha maelfu ya wakazi.

Ukaguzi hasa katika Kaunti ya Mombasa ulionyesha kuwa maeneo ambayo maelfu ya watu walikuwa wakijitokeza kuchukua chakula kutoka kwa tajiri wa Mombasa, Hasmukh Patel, maarufu kama Hasu, yalikuwa yameachwa mwisho wa mwaka wa 2024.

Tajiri huyo aliyefariki pia alianzisha mipango ya chakula katika Kituo cha Sahajanand huko Mtwapa, Kilifi, ambacho kilihudumia watu zaidi ya elfu 60 na kuendesha Shule ya Sahajanand Special School, ambayo inayohudumia watoto 3,000.

Huko Mombasa, inasemekana alitumia shilingi milioni 300 kila mwezi kutoa misaada ya kijamii na alitoa maji safi kwa wakazi wa Kisauni kupitia tanki na kusaidia zaidi ya watu 50,000 waliokuwa na mahitaji.

Kwa mujibu wa Amir, wazo kwamba kampuni hiyo ilikuwa imesitisha mipango ya hisani lilikuwa uvumi wa washindani ili kuharibu kazi nzuri waliyokuwa wakiifanya.

“Unajua watu wengi walidhani kuwa baada ya kifo cha Mkurugenzi wetu Mkuu Hasu, mipango hii itaenda naye, lakini hiyo sio kweli kwa sababu mipango yetu bado inaendelea na kila kitu kiko sawa.” Alisema Amir.

Alihimiza wakazi kuombea kampuni za marehemu Hasu na wanawe ziweze kuongeza mipango ya kusaidia jamii akisema kwamba kampuni ya Mombasa Cement ndiyo pekee pekee inayotekeleza shughuli za kusaidia jamii zinazogharimu mamilioni ya pesa kote nchini.

Amir aliorodhesha baadhi ya mipango ambayo wametekeleza awali kama ujenzi wa kuta za vituo vya polisi, magereza, shule na hospitali.

Kulingana naye, wanashirikiana na magavana Gideon Mung’aro wa Kilifi na mwenzake wa Mombasa, Abdulswamad Sheriff, viongozi wote waliochaguliwa na viongozi wa jamii ili kutambua maeneo yanayohitaji msaada.

Siku moja baada ya mazishi ya Patel, msaidizi wake binafsi, Imtiaz Sayani, alitangaza kuwa familia na viongozi wangezungumzia mipango ya kutoa chakula.

Mkuu wa Shule ya Mkwajuni, Charity Mapenzi, alishukuru Mombasa Cement kwa kuboresha miundombinu yote shuleni.

“Leo tumepokea shule mpya kwa kumbukumbu ya Hasu wa Mombasa Cement na wamekarabati madarasa yote na kujenga mapya, wameweka taa, kuchimba kisima cha maji na kujenga vyoo 16 kwa ajili yetu,” alisema.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *