Mbivu na mbichi inatarajiwa kubainika mwishoni mwa juma hili wakati wa mechi za mzunguko wa tano, hatua ya makundi, kuwania kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchuano wa kwanza wa raundi hiyo, MC Alger ya Algeria iliwatema nje TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo baada ya kuwalaza bao moja bila mjini Algiers katika kundi A.
Al Hilal ya Sudan itawaalika Yanga kutoka Tanzania katika mechi ya pili ya kundi hilo siku ya Jumapili.
Jumamoi, Mamelodi Sundowns ya Afrika wanaoshikilia nafasi ya pili kundini B watawazuru Maniema ya DR Congo, huku viongozi wa kundi hilo, FAR ya Morocco, wakiwa nyumbani kuwatumbuiza wenzao Raja Casablanca katika derby ya Morocco.
Mabingwa watetezi Al Ahly kutoka Misri watawatembelea Stade Abidjan ya Ivory Coast Jumamosi huku viongozi wa kundi C, Orlando Pirates ya Afrika Kusini, wakiwaandaa CR Belouizdad kutoka Algeria Jumapili.
Katika kundi D, Sagrada ya Angola itakuwa nyumbani kumenyana na Pyramids ya Misri Jumamosi huku viongozi wa kundi Esperance kutoka Tunisia wakiwazuru Djoliba ya Mali Jumapili.