Gavana Sakaja aondolea waandalizi filamu ada kwa kuwa watahusisha wakenya

Marion Bosire
2 Min Read

Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja wa kaunti ya Nairobi ametangaza kwamba amewaondolea ada waandalizi wa filamu iitwayo ‘Mercy’ ambao watatumia sehemu kadhaa za katikati mwa jiji na mtaa wa Korogocho.

Hii ni baada ya waandalizi hao kumzuru Gavana katika afisi yake leo ambapo walimwelezea kwamba watatoa fursa zipatazo elfu moja kwa wakazi wa Nairobi ambao watalipwa.

Kati ya hao elfu 1, mia moja wataigiza huku wengine wakipatiwa majukumu ya waigizaji wa ziada na wahudumu wa maandalizi ya filamu hiyo.

Kando na kuondolewa ada, waandalizi hao pia watapata usaidizi wa aina mbali mbali kutoka kwa serikali ya kaunti ya Nairobi kama vile kufunga barabara watakazohitaji na ulinzi.

Sakaja alifafanua kwamba matumizi ya eneo la katikati mwa jiji na waandalizi hao yatafanyika Jumapili pekee ili kuepuka kutatiza watumizi wengine wa jiji.

Kazi hiyo itaendelea kwa muda wa wiki sita.

Appie Matere wa humu nchini ndiye mtayarishaji mkuu wa filamu hiyo ambayo ni igizo la kitabu ‘Mercy’ kilichoandikwa na Lara Santoro, mzaliwa wa Roma, Italia.

Matere anashirikiana na mtayarishaji filamu aitwaye Emily Atef mzaliwa wa West Berlin, ambaye alisema kupitia Instagram kwamba sasa wako tayari kuanza kuandaa ‘Mercy’ baada ya miezi miwili ya matayarisho.

Filamu ‘Mercy’ inasimulia urafiki kati ya wanawake wawili wwenye tofauti nyingi tu. Mercy wa umri wa miaka 35 mama ya watoto wawili anaolea peke yake anayeishi kwenye mtaa wa mabanda jijini Nairobi na Anna wa umri wa miaka 37 mwanahabari wa asili ya Ireland na Italia, aliyetumwa Kenya mwaka 1999.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *