Rais William Ruto leo amezindua miradi kadhaa ya maendeleo katika eneo la North Rift alipoanza ziara ya siku tatu katika eneo hilo.
Rais alianza ziara yake kwa kuzindua ujenzi wa shule ya Liter Girls High School katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, alipotangaza kuwa serikali imetenga shilingi milioni 100 kwa ujenzi wa madarasa katika eneo hilo la North Rift.
Baadaye Ruto alifungua taasisi ya Kerio Valley Technical & Vocational College na pia chuo cha Matibabu nchini KMTC bewa la Kerio.
Akiwa katika kaunti ya Elgeyo Marakwet Rais Ruto, aliongoza ugavi wa hati za miliki ardhi kwa wakazi 10,000, hatua aliyosema itapunguza mizozo ya kijamii katika eneo hilo.
Pia Ruto alikagua ujenzi wa barabara ya kilomita 30 ya Kapcherop – Kipkundul – Kapyego – Kamelei road, Kibirech kaunti ya Elgeyo Marakwet kabla ya kukagua pia ujenzi wa taasisi ya Kapcherop Technical and Vocational College.
Katika kaunti ya Uasin Gishu Rais alifungua ujenzi wa kituo cha maji eneo la Mois’ Bridge.
Rais anatarajiwa kuendelea na ziara yake kesho katika eneo hilo.