Kenya na Angola zitafanya kazi pamoja ili kuhakikisha shirika la ndege la Kenya Airways linaanzisha tena safari za ndege za moja kwa moja kuelekea Luanda, Angola, kuanzia mwezi Machi mwaka huu.
Haya yalitangazwa baada ya mkutano kati ya Marais William Ruto wa Kenya na João Lourenço wa Angola katika Ikulu ya Rais mjini Luanda leo Jumatano.
Hiyo ni hatua kubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi wa nchi hizo mbili.
Fauka ya hayo, Angola itafanya kazi kuelekea kuondoa mahitaji ya viza kwa Wakenya wanaoitembelea nchi hiyo, ikifuata nyayo zilizochukuliwa na Kenya awali.
“Hatua hii itawawezesha wanataaluma wetu kama vile walimu kuelekea nchini Angola kwa urahisi,” alisema Rais Ruto.
Viongozi hao wawili pia walizungumzia masuala muhimu yanayoliathiri bara la Afrika ikiwemo amani katika Eneo la Maziwa Makuu na uchaguzi uliopangwa kufanywa mwezi ujao wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.
Ruto alimsihi Rais Lourenço kuunga mkono juhudi za Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga kugombea wadhifa huo.
Rais Ruto, aliwasili nchini Angola jana Jumanne akitokea Ghana, alikohudhuria uapisho wa Rais John Mahama,
Aliandamana na Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi na Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru miongoni mwa viongozi wengine.