Kampuni ya sanaa ya Millaz Productions imemuomboleza mwanzilishi wake Xavier Nato aliyeaga dunia Disemba 30, 2024 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Katika taarifa kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook, kampuni hiyo ilichapisha picha za Xavier na kuambatanisha na maneno ya kumsifia.
“Xavier alikuwa zaidi ya mtaalamu mwenye maono; alikuwa moyo wa Kampuni ya Millaz. Shauku yake kwa sanaa, uandishi wa hadithi na ucheshi ilichora sio tu kampuni yetu bali pia jamii nzima ya tamthilia.” ilisema taarifa hiyo.
Chapisho hilo liliendelea kusema kwamba kampuni ya Millaz inajulikana kwa hadithi zake za ujasiri na ucheshi, urithi ambao unatokana moja kwa moja na ustadi wa Xavier.
“Tunapolia kwa huzuni kubwa, tutaendelea kujizatiti kuendeleza maono yake kwa kujitolea, ubunifu na umoja aliotuonyesha.” ilisema taarifa hiyo fupi ya maombolezi.
Mwandishi wake alisema pia kwamba Kumbukumbu ya Xavier inawafariji na kuwatia moyo daima na kwamba watamheshimu kupitia hadithi watakazosimulia na maisha watakayogusa.
Taarifa hiyo ilikamilika kwa kusema, “Tuweke Xavier katika mawazo yetu na sala zetu na tukae imara na kupata faraja kadri tunavyoheshimu maisha yake na urithi wake. Safiri salama, X. Tunakupenda. Salimia Don na Sheldon.”
Xavier anasemekana kuugua maradhi ya figo kwa muda mrefu ambayo yalimsababishia kiharusi kabla ya kuaga dunia.
Kampuni aliyoanzisha ya Millaz Productions huwa inahusika na maandalizi ya maigizo ya jukwaani na mengine.