Rais William Ruto ameondoka nchini leo Jumatatu alasiri kuelekea Ghana ambako atahudhuria kuapishwa kwa Rais mteule wa nchi hiyo John Dramani Mahama.
Mahama alimwalika Ruto kuhudhuria uapisho wake wakati wa ziara yake humu nchini mwezi jana.
Msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed anasema wakati akiwa nchini Ghana, Ruto atafanya mazungumzo na Wakuu wa Nchi na Serikali akiwemo Mahama, akiangazia nyanja muhimu za maslahi ya pande mbili na ushirikiano, ikiwemo biashara, nishati, kilimo na uhusiano wa kidiplomasia.
“Kenya na Ghana zina uhusiano mzuri wa muda mrefu ulioanza wakati wa enzi ya kabla ya uhuru, huku nchi zote zikipata hamasa kutokana na mavuguvugu ya ukombozi wakati wa kupigania uhuru, zikiongozwa na ari ya ukombozi wa bara lote la Afrika,” alisema Mohamed kwenye taarifa.
Aidha, Rais Ruto atatumia ziara hiyo kushinikiza Umoja wa Afrika, AU kufanyiwa mabadiliko yanayolenga kuboresha utenda kazi wake.
Na huku uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC, ukiwa umepangwa kufanyika mwezi ujao, Ruto pia analenga kuishukuru Ghana kwa kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kugombea wadhifa huo.
Raila atamenyama na wagombea wengine wawili kutoka Djibouti na Madagascar kumrithi Moussa Faki ambaye muhula wake wa kuhudumu unakaribia kumalizika.