Tume ya mawasiliano ya Uganda yaani Uganda Communications Commission – UCC ambayo inahusika udhibiti katika mawasiliano, utangazaji na huduma za miundombinu, imeapa kufurusha wasanii wa kimataifa wanaotumia lugha chafu kwenye muziki.
UCC imeahidi pia kusafirisha wasanii kama hao hadi nchi zao ambako watachukuliwa hatua za kisheria.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa UCC Nyombi Thembo, kuna haja ya kulinda wasikilizaji na watazamaji wa Uganda hasa watoto kutokana na maudhui yasiyo na maadili.
“Nilishtuka kufahamu kwamba hafla moja iliyoandaliwa mwishoni mwa juma ilisheheni maudhui machafu na nikazungumzia hilo na rafiki.” Thembo alisema hayo katika kikao na wanahabari jijini Kampala.
Kulingana naye, maonyesho kwenye hafla hiyo yalifanana yale ya Sodoma na Gomorrah akisema ipo haja ya kuweka masharti makali ya kudhibiti burudani.
Thembo aliongeza kusema kwamba watashirikiana na mashirika ya ujasusi, kushtaki wasanii wenye lugha chafu wa kimataifa kwenye nchi zao na kuwajibisha waandalizi wa matamasha yao.
Mkurugenzi huyo alishikilia uamuzi wa tume wa kupiga marufuku muziki wenye maudhui yanayokiuka maadili wa msanii Yasin Mukasa maarufu kama Lil Pazo na Gereson Wabuyi maarufu kama Gravity Omutujju.
Alisisitiza kwamba marufuku itagusa tu nyimbo zenye maneno machafu kama vile enkudi, Dooze na Okwepiicha.
Hata hivyo msako dhidi ya maudhui yanayokiuka maadili kwenye burudani nchini Uganda umeibua mjadala kuhusu uhuru wa kujieleza.
Tume hiyo ya mawasiliano inasisitiza kwamba kushabikia maudhui kama hayo kunakiuka sheria za Uganda na kuhujumu maadili ya kitamaduni ya taifa hilo.