Mwimbaji wa Taarab maarufu nchini Tanzania Khadija Kopa amemzomea Maimartha Jesse kwa madai ya kumsema na kumdhalilisha binti yake Zuchu.
Hii ni baada ya Maimartha aliyekuwa akizungumza na wanahabari wa mitandaoni kudai kwamba Zuchu hapendi watu wa familia ya mpenzi wake Diamond Platnumz na kamwe hana heshima kwao.
Kopa alimpigia simu Maimartha mawasiliano ambayo Mai alirekodi na kuyaonyesha kwenye kipindi chake cha mitandaoni ambapo alimwonya akome kumsema mwanawe kila mara.
Katika mawasiliano hayo ya simu, Kopa alitaka kujua alikotoa taarifa kuhusu mwanawe zuchu ili amkabili moja kwa moja.
“Nimechoka! Hamuishi kumsimanga na kumsema mwanangu kila siku maneno machafu. Mwanangu hana dosari yoyote!Nimemlea kwa nidhamu anaheshimu watu wazima wakubwa na wadogo.” alifoka Khadija.
Mama huyo alisema kwamba yuko tayari kununua ugomvi na kwamba yuko tayari kuwaendea hewani wanaomdhalilisha mwanawe Zuchu.
Cha ajabu ni kwamba Maimartha alisema kwamba yeye na Khadija ni marafiki na watani wa muda mrefu akisema kwamba anachoendelea kufanya ni kazi kama ambayo Khadija hufanya anapoimba jukwaani.
Maimartha anasisitiza pia kwamba kila ambalo yeye hulisema mitandaoni ni la kweli na kwamba Kopa alikasirika kwa sababu kawaida watu hawapendi mambo yao ya ndani yafichuliwe kwa umma.
Katika udaku wake Maimartha wa Mai Tv alidai kwamba hatua ya kupeleka posa kwa kina Zuchu ilisitishwa kwani wanafamilia wa Diamond hawampendelei Zuchu kuwa mkwe wao.
Diamond Platnumz amekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki mwenza Zuchu wengi wakitarajia wataoana lakini bado.
Platnumz ameripotiwa kuwa na mahusiano mengine ya kimapenzi na wanawake wengine kipindi ako na Zuchu kama vile mrembo kwa jina Rita na mhusika mwenzake wa kipindi cha Young Famous and African cha Netflix Fantana.
Alionekana akimbusu Fantana kwenye kipindi hicho hatua iliyomghadhabisha Zuchu huku akiambia Fantana kwamba Zuchu ni mwanamuziki aliyesajiliwa kwenye kampuni yake tu.
Katika mkutano mkuu wa kitaifa wa chama cha CCM, Diamond alimwambia Nandy kwamba atafanya harusi kabla ya Ramadhan ambayo inatarajiwa kuanza mwezi Machi na kufikia sasa hakuna dalili.