Mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati ameaga dunia.
Chebukati alifariki jana Alhamisi jioni wakati akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi.
Alikuwa na umri wa miaka 63.
Chebukati alisimamia IEBC kwa kipindi cha miaka 6 baada ya kuteuliwa kwenye wadhifa huo mwezi Januari mwaka 2017.
Aliondoka kwenye wadhifa huo mwezi Januari mwaka 2023 baada ya kusimamia chaguzi tata za mwaka 2017 na 2022.
Chebukati na makamishna Prof. Abdi Guliye na Boya Molu ndio pekee waliohudumu kwa kipindi cha miaka sita.
Makamishna wengine ambao ni Juliana Cherera, Francis Wandera, Irene Masit na Justus Nyang’aya (maarufu kama Cherera 4) walijiuzulu kabla ya kumalizika kwa muhula wao wa kuhudumu.
Wanne hao walichukua hatua hiyo kutokana na utata uliogubika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Mchakato wa kutafuta mrithi na Chebukati na waliokuwa makamishna wa tume hiyo kwa sasa unaendelea.
Chebukati alikuwa mwanasheria aliyejizolea tajiriba ya miaka 37 katika masuala ya sheria nchini.
Rais William Ruto na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ni miongoni mwa walioomboleza kifo chake.