Mwanamuziki wa Marekani A$AP Rocky aliondolewa lawama kwenye mashtaka mawili ya uhalifu yaliyokuwa yakimkabili, na mahakama moja huko Los Angeles Jumatatu.
Uamuzi huo wa mahakama unakamilisha mchakato mrefu wa kisheria ambao A$AP ambaye jina lake rasmi ni Rakim Mayers, amepitia kufuatia kisa kilichohusisha bunduki mwaka 2021 huko Hollywood.
Kundi la waamuzi wa kesi hiyo liliafikia uamuzi huo baada ya majadiliano ya siku kadhaa, huku upande wa utetezi ukisema kwamba A$AP alichukua hatua ya kujikinga.
Punde aliposikia uamuzi wa kutompata na hatia, A$AP Rocky alijawa na furaha na kumrukia mpenzi wake na mzazi mwenza Rihanna na kumpiga pambaja.
Alishukuru mawakili wake na kuhutubia mahakama kwa kifupi ambapo alisema anashukuru kwani ukweli ulisikika.
Wakati vikao vya kesi hiyo vilikuwa vikiendelea, mpenzi wa Mayers mwanamuziki Rihanna alisimama naye huku akihudhuria baadhi ya vikao hivyo.
Rihanna amekuwa wa msaada sana kwa A$AP Rocky na pamoja wana watoto wawili. Uwepo wake mahakamani wakati wa uamuzi huo kutolewa ulidhihirisha mapenzi kati yao.
Hatua ya kuondolewa lawama sasa inampa mwanamuziki huyo fursa ya kurejelea kazi yake na maisha yake ya kawaida.