Kenya leo Jumatatu imejiunga na ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kupambana na Ufisadi Duniani.
Hafla ya kuadhimisha siku hiyo inafanyika katika Chuo Kikuu cha Strathmore jijini Nairobi.
Mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC Dkt. David Oginde, Balozi wa Umoja wa Ulaya na vile vile Balozi wa Uingereza humu nchini ni miongoni wanaohudhuria hafla hiyo.
Aidha, washikadau mbalimbali kutoka kwa taasisi za umma, kibinafasi, mashirika ya kijamii na ya kidini wanahudhuria.
Siku ya Kupambana na Ufisadi Duniani huadhimishwa ili kuangazia hatua zilizopigwa dhidi ya ufisadi, changamoto zilizojitokeza katika kupigana na uovu huo, mafunzo yaliyopatikana na marekebisho yanayopaswa kufanywa ili kuhakikisha vita dhidi ya ufisadi vinafanikiwa.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni, “Kuungana na Vijana dhidi ya Ufisadi: Kuratibu Uadilifu wa Kesho.”
EACC inasema kaulimbiu hiyo ni ishara tosha ya umuhimu wa vijana katika kusaidia kuimarisha vita dhidi ya ufisadi wakati wakihamasisha uadilifu katika jamii.
Maadhimisho hayo yamekuja wakati ambapo kumekuwa na madai ya kukithiri kwa visa va ufisadi nchini.
Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi amenukuliwa akisema Kenya hupoteza zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa mwaka kutokana na ufisadi.
EACC imekuwa ikitoa wito kwa Wakenya kukaa macho na kuhakikisha wanaripoti visa vya ufisadi ili kuhakikisha vita dhidi ya uovu huo nchini vinafanaikiwa.