Waziri Barasa: Wakenya sasa wanapata huduma bora za matibabu kupitia SHA

radiotaifa
1 Min Read
Deborah Barasa - Waziri wa Afya

Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa amesema Wakenya kwa sasa wanapata huduma bora za afya ya msingi bila malipo katika hospitali za umma kupitia mpango wa Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA. 

Huduma hizo pia zinapatikana katika hospitali za kibinafasi na za  kidini zilizotia saini mikataba na serikali.

Dkt. Barasa anasema kufikia sasa, Wakenya zaidi ya milioni 15.2 wamejisajili kwenye mpango huo.

“Wizara ya Afya bado imedhamiria kutoa huduma bora za afya na za gharama nafuu kwa Wakenya wote,” amesema Dkt. Barasa leo Jumatatu alipokutana na washikadau wa hospitali za kidini jijini Nairobi.

Kufikia sasa, hospitali 8,336 zimetia saini mikataba na serikali chini ya mpango huo huku hospitali 5,210 zikiwa ni za serikali, 319 za kidini na 2,807 za kibinafsi.

Waziri amesisitiza wajibu muhimu unaotekelezwa na hospitali za kidini katika utoaji huduma hasa vijijini na maeneo yasiyokuwa na miundombinu inayohitajika.

Wakati wa mkutano huo, washikadau walijadili changamoto zinazotokana na utekelezaji wa mpango wa SHA na namna ya kuzisuluhisha.

Dkt. Barasa amefichua kuwa Wizara yake tayari imezilipa hospitali zinazotoa huduma za afya kwa Wakenya chini ya SHA shilingi bilioni 5.05 huku hospitali za kidini zikilipwa shilingi milioni 938.6 kati ya shilingi hizo.

Share This Article