Millicent Ayuwa maarufu kama Dem wa Facebook amerejelea fani yake ya awali ambayo ni kucheza soka.
Alitambulishwa rasmi kama mmoja wa wachezaji kwenye timu ya Bungoma Queens, walipokuwa wakicheza dhidi ya Zetech Sparks katika mechi ya ligi ya wanawake nchini.
Ayuwa na wenzake waliibuka washindi kwenye mechi hiyo katika uwanja wa michezo wa Dandora, kwa mabao matatu kwa moja.
Dem wa Facebook alihusishwa kama mchezaji wa akiba wa kipindi cha pili.
Kabla ya kuingilia shughuli za kuunda maudhui mitandaoni, Ayuwa aliichezea timu ya wanawake ya Trans-Nzoia Falcons kwa muda wa miaka mitano.
Mwaka 2018 timu hiyo ilishinda kinyang’anyiro cha Chapa Dimba na Safaricom.
Alipoulizwa kuhusu jinsi anapanga kusawazisha muda wake kati ya uandaaji wa maudhui mitandaoni na soka, Dem wa Facebook alijibu kijanja.
“Jinsi wanaume wanaweza kugawa muda wao kati ya wake zao na wanawake wa kando.” alisema Ayuwa huku akimtaka waziri wa michezo Kipchumba Murkomen ampe fursa.
Fursa hiyo ni katika kuwamotisha na kuwanoa makali wachezaji wanaoibuka chini ya mpango wa Talanta Hela.