Waziri wa kilimo Dkt. Andrew Karanja, leo Alhamisi alishiriki mazungumzo na chama cha watengenezaji mbolea hapa nchini, kwa lengo la kuimarisha shughuli za kilimo.
Mkutano huo pia ulikusudia kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta ya kibinafsi katika kufanikisha shughuli za kilimo hapa nchini.
Waziri huyo alielezea jukumu muhimu linalotekelezwa na sekta ya kibinafsi katika miradi ya kilimo, hususan usambazaji wa mbolea ya gharama nafuu.
“Lengo letu sio kuvuruga sekta ya kibinafsi, lakini kulishirikisha katika mipango yetu,” alisema waziri huyo.
Aidha waziri huyo alisema mipango inaendelea kuhakikisha kila mmea unakuwa na aina yake ya mbolea na kujumuishwa kwenye mpango wa mbolea za bei nafuu, ili wakulima wanapate mbolea ifaayo kuimarisha uzalishaji.
“Tunajizatiti kuhakikisha tunazalisha mbolea hapa nchini, ili kupunguza utegemezi kutoka nje,” aliongeza waziri huyo.
Dkt. Karanja aliwahakikishia wakulima kuwa matayarisho yamekamilika huku msimu wa mvua za masika mwaka 2025 ukitarajiwa.
“Mbolea za gharama nafuu zitawasilishwa katika maghala ya halmashauri ya nafaka na mazao nchini NCPB kufikia mwezi Januari mwaka 2025,” alidokeza waziri huyo.