ACK yaungana na Kanisa Katoliki katika kuikosoa serikali

Martin Mwanje
2 Min Read

Kanisa la Kiangilikana nchini Kenya, ACK limeelezea kuunga mkono msimamo wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki ambao wiki iliyopita walishutumu vikali serikali ya Kenya Kwanza kwa kuzembea kazini. 

Katika kuinyoshea serikali kidole cha lawama, Maaskofu wa Kanisa Katoliki walilalamikia madeni chungu nzima inayodaiwa iliyokuwa Hazina ya Taifa ya Bima ya Afya, NHIF na hulka ya utawala wa sasa kutotimiza ahadi ilizotoa kwa Wakenya.

Aidha, miongoni mwa masuala mengine, Maaskofu walilalamikia visa vya utekanyi nyara vinavyoripotiwa nchini, ukiukaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza kwa mujibu wa katiba.

“Sisi ACK, tunaiunga mkono kikamilifu taarifa ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki. Tunaamini kuwa serikali bado haijaleta mabadiliko na kuielekeza nchi katika mwelekeo unaofaa,” alisema Askofu Mkuu wa ACK Jackson Ole Sapit wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumatatu.

“Kuwaita viongozi wa kidini majina au kupuuzilia mbali taarifa ya Maaskofu kama inayopotosha, isiyo sahihi na ya uongo ni hatua isiyokuwa na uaminifu.”

Kulingana na Ole Sapit, Maaskofu hao walikuwa tu wakizungumza msimamo wa Wakenya na ukweli wa hali ya mambo yalivyo nchini.

“Hakuna kiwango cha mashambulizi au matishio kitalizuia kanisa dhidi ya kushutumu maovu na kuwaelezea viongozi ukweli,” alibainisha Askofu Sapit.

Matamshi yake yanakuja wakati viongozi wa kisiasa wanaoegemea serikali ya Kenya Kwanza wamewakosoa vikali Maaskofu hao wakiwataka kutoa suluhu kwa matatizo yanayolikumba taifa badala ya kuwa tu wakosoaji.

 

 

 

Share This Article