Kituo cha kuwatunza watoto kujengwa Busia

Martin Mwanje
1 Min Read

Serikali ya kaunti ya Busia imekabidhi ekari moja ya ardhi kwa Kituo cha Ushirikiano wa Jinsia na Maendeleo (CCGD). 

CCGD ambalo ni shirika lisilokuwa la serikali linatarajiwa kujenga kwenye ardhi hiyo kituo cha kuwatunza watoto.

Kituo hicho kitakachojengwa katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Busia kinatarajiwa kutoa huduma za hali ya juu kwa wakazi.

Aidha kinatarajiwa kuhudumia wanawake zaidi ya 1,000 katika kaunti hiyo kwa kuwawezesha kuwaacha watoto wao katika eneo salama wakati wakishughulikia masuala mengine.

Wawakilishi wa CCGD Grace Kathau na Sharon Ngaira wameelezea dhamira yao ya kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

Ngaira amesema kuwa kituo hicho kitafanya kazi kama taasisi ya umma kwa kutumia modeli ya maendeleo inayoungwa mkono na uongozi thabiti kutoka kwa serikali ya kaunti ya Busia.

Afisa Mkuu wa kaunti ya Busia anayesimamia Masuala ya Jinsia Pasilisa Barasa amesema kuwa kituo hicho kitawahamasisha wanawake hasa wasichana walio na watoto kwa kuwapa fursa ya kurejea shuleni au kushiriki shughuli zingine za kuwaletea mapato.

TAGGED:
Share This Article