Chuo kikuu cha Yale kimetangaza ujio wa kozi kuhusu mwanamuziki Beyoncé Knowles-Carter mwaka ujao.
Kozi hiyo kwa jina “Beyoncé Makes History: Black Radical Tradition, Culture, Theory & Politics Through Music” itafunzwa na mkufunzi wa chuo hicho wa maswala ya Afrika na Amerika Profesa Daphne Brooks.
Itaangazia athari za kitamaduni za mwanamuziki huyo nyota na wanafunzi wataangazia jinsi Beyonce kupitia kwa kazi zake alihamasisha na kuhusisha umma katika mafundisho ya kijamii na kisiasa.
Miziki ya Beyonce itatumika pakubwa katika kozi hiyo kama chombo cha kufundisha kuhusu wajuzi wengine wamarekani weusi kama vile Toni Morrison na Frederick Douglass.
Hii sio mara ya kwanza mwanamuziki maarufu anaangaziwa kama kozi katika taasisi za masomo ya juu nchini Marekani.
Taasisi ya Clive Davis ya muziki chini ya chuo kikuu cha New York, ilitoa kozi kuhusu Lana Del Rey iliyofunzwa na mwanahabari na mwandishi wa vitabu Kathy Iandoli.
Taylor Swift aliwahi kuangaziwa katika chuo kikuu cha Texas na katika taasisi ya Clive Davis ya chuo kikuu cha New York.
Mume wa Beyonce Jay Z aliangaziwa katika chuo kikuu cha Georgetown kwenye kozi iliyopatiwa mada “Sociology of Hip-Hop: JAY-Z” kati ya wanamuziki wengine.