Ufafanuzi kuhusu miradi iliyokwama katika kaunti ya Kwale

Marion Bosire
2 Min Read
Gavana wa Kwale Fatuma Achani.

Serikali ya kaunti ya Kwale imefafanua kuhusu kuwepo kwa miradi iliyokwama katika eneo hilo.

Kucheleweshwa kwa miradi hiyo kulingana na serikali ya Kwale, kunatokana na kuchelewa kwa fedha za magatuzi kutoka kwa serikali kuu.

Miradi iliyokwama ni pamoja na soko la Kombani, barabara ya Kona Musa Mabokoni, kiwanda cha matunda pamoja na makazi ya gavana.

Akihutubia wanahabari katika afisi za kaunti ya Kwale, wanachama wa kamati kuu ya kaunti wakiongozwa na anayesimamia masuala ya fedha Bakari Sebe walielezea miradi inayokamilishwa katika muda wa mwaka mmoja na ile inayotekelezwa katika awamu kadhaa.

Kulingana na Sebe miradi yote, ile inayotekelezwa mara moja au kwa awamu inapendekezwa na wakazi kwa njia ya kushirikisha umma.

Miradi ya awamu ambayo imekamilika inajumuisha taasisi ya mafunzo kwa walimu ya Kwale. bwawa la Mwakalanga, uwanja wa michezo wa Kwale, kituo cha matibabu ya saratani cha Msambweni na ukarabati wa hospitali ya rufaa ya Msambweni.

Mwanachama wa kamati kuu anayehusika na utalii Michael Mutua alikanusha madai kwamba milioni 600 zimetumika kufikia sasa kwa kiwanda cha matunda ilhali hakijakamilishwa.

“Kufikia sasa tumetumia milioni 206 pekee kwa awamu ya kwanza na ya pili ambazo zimekamilika na kuwasilishwa kwa serikali.” alisema Mutua. Akiongeza kwamba mkataba wa mwanakandarasi ulisitishwa baada ya kubainika kufanya kazi duni.

Kuhusu soko la Kombani Mutua alisema ilifunguliwa na kuanza kutumika ila mwanakandarasi alikwenda mahakamani akidai kukosewa na hivyo waliokuwa wakitumia soko hilo wakatimuliwa na agizo la mahakama.

Makazi ya gavana alisema gavana anaishi kwenye nyumba yake binafsi na hakuna pesa zimetumika kumlipia kodi ya nyumba.

Mwanasheria wa kaunti hiyo Salim Gombeni alilaumu wanakandarasi ambao wamekuwa wakikimbilia mahakama kandarasi zao zinapositishwa.

Msimamizi wa masuala ya barabara katika kamati kuu ya kaunti ya Kwale Joto Mwachirumbi alisema ujenzi wa barabara ya Kona Musa -Mabokoni umechelewa kufuatia kusitishwa kwa kandarasi.

Wanachama hao wa kamati kuu ya kaunti ya Kwale wanawataka wakazi kuhusika katika mchakato wa kuandaa bajeti kupitia vikao vya kushirikisha umma ili kujifahamisha kuhusu miradi iliyoanzishwa na serikali ya kaunti.

Share This Article