Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, amesema Kenya na Botswana zinaimarisha ushirikiano katika sekta za Mabadiliko ya Tabia Nchi, Utalii, na biashara ya kahawa na majani chai.
Kupitia mtandao wa X leo Jumamosi, Kindiki alisema alishauriana na Rais wa Botswana Duma Gideon Boko aliyeapishwa Jana Ijumaa na kukubaliana kuhusu ustawishaji wa ufugaji ng’ombe wa nyama, ukuzaji wa kilimo cha bustani na maua, uchimbaji madini, usimamizi wa vyama vya ushirika, amani, usalama na utulivu wa kikanda.
“Kenya inaitambua Botswana kama mshirika katika maswala ya ukuaji wa uchumi barani humu, amani, elimu, afya na nishati safi,” alisema Kindiki.
Alibainisha kuwa mataifa haya mawili yamebadilishana uzoefu katika nyanja za siasa, demokrasia, maendeleo na biashara, tangu enzi za kupigania uhuru.
Kulingana na naibu huyo wa rais, kwa sasa zaidi ya raia 1,200 wa Kenya wanaishi na kufanya kazi nchini Botswana, huku serikali ya Kenya ikiridhia makaribisho wanayopokea wataalamu wa Kenya ambao kwa muda wamechangia katika kuanzisha mifumo ya utawala na elimu nchini Botswana.
Wakati wa mazungumzo hayo, Kindiki pia aliwasilisha ombi la Rais Ruto kwa Rais Duma Boko, la kuunga mkono kuteuliwa kwa Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika ‘AUC’.