Jopo la majaji watatu leo Jumanne, linatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu uhalali wa mchakato wa kumvua Rigathi Gachagua wadhifa wa Naibu Rais.
Rigathi Gachagua alifika Mahakamani Ijumaa iliyopita, kupinga utamuzi wa bunge la Seneti kumuondoa mamlakani, baada ya bunge hilo kumpata na makosa matano kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake.
Macho yote sasa yameelekezwa kwa Majaji Eric Ogola, Antony Mrima na Freda Mugambi, huku wakitarajiwa kusikiliza ombi hilo ambalo pia linapinga kuapishwa kwa Prof. Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.
Baada ya kutimuliwa kwa Gachagua na bunge la Senate, Rais William Ruto alimteua Waziri wa usalama wa taifa Prof. Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais mpya, na jina lake kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali.
Gachagua alijaribu mara kadhaa kusimamisha michakato ya kumuondoa mamlakani bila kufua dafu, huku akiwasilisha takriban kesi 26.