Rais William Ruto ameahidi kwamba serikali itaendelea kupiga jeki kilo humu nchini ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha.
Akizungumza alipoongoza sherehe za siku ya mashujaa katika kaunti ya Kwale, Rais alisema serikali inaendelea kuinua sekta ya kilimo na kuleta mabadiliko katika viwango vyote vya uzalishaji.
Alitaja uvuvi na ukuzaji samaki, kilimo cha maua, cha vyakula, ufugaji na maendeleo mengine ya sekta hiyo muhimu.
“Uwekezaji unatekelezwa ili kuinua utengenezaji na upatikanaji wa pembejeo bora, kutoa huduma bora za ushauri, kupunguza hasara ya baada ya mavuno na kuongezea wazalishaji mapato.” alisema Rais kwenye hotuba yake.
Alisema pia kwamba wamekamilisha shughuli ya kuagiza mbolea ya bei nafuu ambayo bei yake alisema itasalia kuwa shilingi 2500 kwa kila gunia la kilo 50 kama ilivyokuwa awali.
Kiongozi wa nchi alielezea kwamba juhudi zinazotekelezwa na serikali zinalenga kuhakikishia wazalishaji faida kupitia kwa kukusanya bidhaa, kuongeza thamani ya bidhaa na kuuza nje ya nchi.