Itakuwa ni zamu ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kujitetea dhidi ya mashtaka 11 yaliyowasilishwa dhidi yake katika Bunge la Seneti leo alasiri.
Gachagua anatarajiwa kujitetea katika bunge hilo kuanzia majira ya saa 8:30.
Hii ni baada ya pande zote kurushiana cheche kali za kisheria kuhusiana na hoja maalum iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse ikitaka Gachagua aondolewe kwenye wadhifa huo.
Gachagua anatarajiwa kuelezea upande wake wa mambo kuhusiana na hoja hiyo iliyoungwa mkono na wabunge 281 katika Bunge la Taifa siku chache zilizopita.
Ikiwa Maseneta 45 kati 67 wataiunga mkono, basi itakuwa rasmi Naibu Rais amepoteza wadhifa huo.
Ikiwa Maseneta 23 wataipinga, basi Gachagua atakuwa na kila sababu ya kutabasamu kwani atakuwa amenusurika.
Jana Jumatano, Mutuse alikuwa na wakati mgumu kutetea mashtaka 11 aliyowasilisha dhidi ya Naibu Rais huku timu ya mawakili wa Gachagua ikifanya kila iwezalo kudhihirisha ni ya uongo.
Maseneta wanatarajiwa kuipigia kura hoja hiyo majira ya saa mbili leo usiku katika hatua itakayoamua hatima ya Gachagua kisiasa.