Wahudumu wa afya ya umma wasiokuwa na vyeti vya kuhudumu huenda wakasimamishwa kazi.
Onyo hilo limetolewa na Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni.
Muthoni amesema wahudumu hao wanafaa kufuata masharti yote ya kuhudumu kutoka kwa wizara hiyo, ambayo yanajumuisha wao kuwa na vyeti vya kuhudumu.
Akizungumza mjini Machakos baada ya kukutana na wahudumu hao, Muthoni anasema wengi wa wahudumu wa afya ya umma wametelekeza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi shuleni na katika maeneo ya kuuza nyama pamoja na vyakula kwa lengo la kubaini hali ya usafi ya maeneo hayo na ni wakati sasa wanafaa kuzinduka.
Kulingana naye, wengi wa wafanyabiashara wa vyakula wanauza vyakula hivyo bila leseni na kuzingatia kanuni za afya. Anasema hali imechangia kuongezeka kwa magonjwa yanayotokana na mazingira machafu kikiwemo kipindupindu.
Katibu Muthoni anasema wahuhudumu wa afya ya jamii laki moja kwa ushirikiano na maafisa wa afya ya umma watahakikisha wametoa mchango mkubwa katika kuzuia maradhi kama hayo.
Wakati wa ziara yake mjini Machakos, Muthoni pia alizuru hospitali ya Machakos Level 5 na kuthibitisha kuwa wengi wa wakazi wamesajili kwenye bima mpya ya afya ya jamii ya SHIF.
Amewashauri Wakenya kujitokeza kwa wingi kujisajili kwenye bima hiyo kwa sababu asilimia mia moja watakuwa wakipata huduma za afya ikilinganishwa na asilimia ishirini waliokuwa wakipata huduma kwenye bima ya zamani ya NHIF.
Tayari wakazi 147, 050 katika kaunti ya Machakos wamejisajili kwenye bima ya SHIF.