Kikao cha Maseneta wote kitaamua hatima ya Naibu Rais Rigathi Gachagua wiki ijayo.
Hii ni baada ya Maseneta leo Jumatano asubuhi kukataa pendekezo la kubuni kamati maalum ya Maseneta 11 kuchunguza mashtaka dhidi ya Gachagua.
Bunge la Seneti sasa litaandaa kikao cha kusikiliza mashtaka hayo siku za Jumatano na Alhamisi wiki ijayo.
“Namuagiza; karani kutoa mwaliko wa kufika mbele ya Bunge la Seneti leo. Bunge lote la Seneti litachunguza suala hilo Oktoba 16 na 17,” alisema Kingi wakati wa kikao cha leo Jumatano asubuhi.
Jana Jumanne, Bunge la Taifa lilipiga kura kuunga mkono hoja maalum ya kumuondoa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Hoja hiyo yenye mashtaka 11 iliwasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Wabunge 281 waliunga mkono hoja hiyo huku 44 wakiipinga.
Mbunge mmoja hakupiga kura.