Naibu Rais Rigathi Gachagua, amedokeza kuwa masaibu yanayomkumba ya kutaka aondolewe mamlakani, yanatokana na hulka yake ya kuwa msema ukweli.
Akihutubia taifa Jumatatu usiku katika makazi yake rasmi ya Karen, Gachagua alisema kamwe hawezi kimya huku mambo yakienda kombo, swala ambalo haliwafurahishi wakosoaji wake.
“Kwa sababu mimi ni msema ukweli, sitanyamaza mambo yakienda kombo. Utekaji nyara na mauaji ya kiholela ni kinyume cha katiba,” alisema Gachagua katika mkutano na waandishi wa habari.
Gachagua alisema tangu walipoingia madarakani pamoja na Rais William Ruto, ametekeleza majukumu aliyopatiwa na Rais Ruto kwa uadilifu na kwa bidii na hajapokea malalamishi kutoka kwa Rais kuhusu utepetevu wa majukumu yake.
“Rais William Ruto hajalalamika kwangu kuwa nimemhujumu. Iwapo alimwambia mbunge Mutuse, ningependa kujua,” alisema Gachagua.
Alisema amekuwa mwaminifu kwa Rais William Ruto na kwamba hatakubali juhudi zake kuvurugwa.
Gachagua alisema atafika mbele ya bunge la taifa leo Jumanne saa kumi na moja jioni, kujitetea dhidi ya madai yaliyowasilishwa dhidi yake.
Madai hayo ni pamoja na ukiukaji wa katiba, utovu wa maadili, ufisadi, kumheshimu Rais na kumtishia jaji mmoja miongoni mwa mengine.