Bunge la taifa limetoa ratiba ya kupokea maoni ya umma kuhusu hoja iliyowasilishwa katika bunge hilo, ya kumbandua Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Kulingana na ilani iliyochapishwa na karani wa bunge la taifa Samuel Njoroge, maoni hayo yanaweza tolewa kupitia mtandano kwa anwani; impeachment@parliament.go.ke kufikia Oktoba 5, 2024 saa kumi na moja jioni.
Wakenya pia wanaweza toa maoni kupitia vituo vilivyotangazwa hapo chini, kufikia Oktoba 4,2024 saa kumi na moja jioni.
Hatua hiyo inajiri baada ya wabunge 291, kutia saini hoja ya kumuondoa mamlakani naibu rais, na kuwasilisha hoja hiyo katika bunge la taifa Jumanne asubuhi.
Hoja hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, inaorodhesha maswala kumi dhidi ya Gachagua, yakiwa ni pamoja na ukiukaji wa katiba, uhalkifu wa kiuchumi,ulanguzi wa fedha na utovu wa maadili, miongoni mwa maswala mengine.
Mbunge huyo alisema ametoa ushahidi wa kutosha kuunga mkono kubangudliwa kwa Naibu huyo wa Rais.
“Kwa muda wa miaka miwili, Rigathi Gachagua amejipatia shilingi bilioni 5.2 kutokana na shughuli za ufisadi na ulanguzi wa pesa,” ilisoma sehemu ya hoja hiyo.
Mjadala kuhusu hoja ya kumbandua mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua, utaanza Jumanne wiki ijayo huku Naibu huyo wa Rais akitarajiwa kufika mbele ya bunge baina ya saa kumi na moja jioni na saa moja usiku.
Akilielekeza bunge kuhusu mchakato mzima, spika wa bunge la kitaifa Moses wetangula alisema bunge litakosa vikao vyake Jumatano alasiri ili kuupa nafasi umma kuchangia suala hilo kuanzia Ijumaa tarehe 4 mwezi huu wa Oktoba.