Wahudumu wa afya kaunti ya Meru wahimizwa kusitisha mgomo

Tom Mathinji
1 Min Read
Wahudumu wa afya kaunti ya Meru washiriki mgomo.

Katibu wa kaunti ya Meru Dkt Kiambi Athiru, ametoa wito kwa wahudumu wa afya katika kaunti hiyo kusitisha mgomo wao, akihakikisha kuwa serikali ya kaunti hiyo inashughulikia maswala yao.

Akizungumza afisini mwake Jumanne, Dkt. Athiru alidokeza kuwa mgomo huo umesambaratisha huduma za matibabu katika vituo vya afya vya umma, huku wakazi wakihangaika kutoka na ukosefu wa huduma hizo.

Kulingana na katibu huyo, serikali ya kaunti hiyo imetenga shilingi milioni 211, ili kuwapandisha vyeo wahudumu hao wakiwemo maafisa wa kliniki ambao watapokea barua zao za kupandishwa vyeo Septemba 13, 2024.

Wahudumu hao wa afya ambao wameshiriki mgomo kwa muda wa mwezi mmoja sasa, wameapa kutorejea kazini hadi matakwa yao yatakaposhughulikiwa kikamilifu.

Mwenyekiti wa chama cha madaktari na wataalam wa meno KMPDU eneo la Mashariki mwa nchi Denis Mugambi, alidokeza kuwa wahudumu wengi wa afya wamestaafu bila ya nafasi zao kujazwa.

Aidha alikanusha madai kwamba mgomo huo umechochewa kisiasa, akisema kuwa Gavana wa kaunti hiyo Kawira Mwangaza wakati wa kamepeni za uchaguzi mkuu mwaka 2022, aliwaahidi kuwa atashughulikia changamoto zinazoghubika wahudumu hao wa afya ikiwa ni pamoja na kupandishwa vyeo, kuajiriwa kwa wahudumu zaidi na kuwasilishwa kwa matozo yao katika taasisi husika.

TAGGED:
Share This Article