Hazina ya kimataifa kuhusu ustawi wa kilimo (IFAD), itafadhili miradi ya taifa hili ya mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa chakula na usawa wa mapato, kwa kitita cha shilingi bilioni 16.3.
Ufadhili huo ni sehemu ya mpango jumuishi wa usimamizi wa mali asili, ambao ungali unajadiliwa.
Mpango huo unalenga kushughulikia changamoto kuu zinazokabili Kenya, hasaa miongoni mwa makundi maalum kama vile wanawake, vijana na watu wanaoishi na ulemavu.
Ujumbe wa Kenya ukiongozwa na katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh na mwenzake wa fedha Dkt.Chris Kiptoo, unaendelea kushiriki meza ya mazungumzo na kundi la IFAD, ambalo linaongozwa na mkurugenzi wake wa hapa nchini Mariatu Kamara.
Mradi huo unatarajiwa kutumia jumla ya shilingi bilioni 32.2, huku fedha zilizosalia zikitolewa na serikali ya Kenya na washirika wake wa maendeleo.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Ronoh aliangazia umuhimu wa majadiliano hayo katika kutimiza lengo la kubadilisha maisha ya walengwa na kuimarisha usalama wa chakula.
“Pamoja tumejitolea kuangamiza umaskini na kuboresha maisha ya wakenya, hususan katika maeneo ya mashinani ambakomiradi hii inahitajika zaidi.” alisema Dkt. Ronoh.
Dkt. Ronoh alitambua umuhimu wa ufadhili wa IFAD, katika kupija jeki ajenda ya maendeleo ya taifa hili.