Walimu wanaogoma wa shule za sekondari na vyuo nchini huko Thika kaunti ya Kiambu, waliwaondoa wenzao waliokuwa wamefika kazini katika shule ya upili ya wasichana ya Chania.
Wakiongozwa na viongozi wa chama chao KUPPET walimu hao waliandamana hadi lango la shule hiyo wakasalia huko wakiimba nyimbo zao za utetezi hadi baadhi ya wenzao wanaofanya kazi kwenye shule hiyo wakajiunga nao.
Hawakuweza kuingia shuleni humo kwa sababu lango lilikuwa limefungwa na linalindwa na maafisa wa polisi waliojihami. Walijibizana na maafisa hao kidogo kabla ya kuendelea na maandamano katika barabara za mji wa Thika.
Mwenyekiti wa tawi la kaunti ya Kiambu la chama cha KUPPET Daktari Rose Kiiru alisema chama hicho kiliamua kususia maagizo ya mahakama ya ajira ya kurejea kazini baada ya mwajiri wao TSC kukosa kutii maagizo ya mahakama kuu ya kukoma kuwatoza ada ya nyumba za gharama nafuu.
Kiiru alisema pia kwamba agizo la mahakama lilitolewa likiwa limechelewa wakati ambapo tayari walikuwa wameanza mgomo baada ya tume hiyo ya kuajiri walimu TSC kukosa kuafikiana na viongozi wa KUPPET.
Mgomo huo kulingana naye umelemaza masomo katika shule za upili huku akiwataka wazazi waliorejesha wanao shuleni wawachukue nyumbani kwa usalama wao.
Alisema mgomo utaendelea hadi matakwa yao yatekelezwe na serikali.