Watu wapatao 70 waliachwa na majeraha mbali mbali baada ya treni waliyokuwa wakisafiria kuhusika kwenye ajali huko Kigoma nchini Tanzania.
Katika taarifa shirika la reli la Tanzania – TRC lilielezea kwamba treni ya abiria nambari Y14 ambayo kichwa chake ni nambari 9002 ilipata ajali kati ya kituo cha treni cha Kazuramimba na Uvinza katika mkoa wa Kigoma.
Ajali hiyo iliyoathiri mabewa 12 ya abiria, bewa moja la mizigo na bewa moja la breki inaripotiwa kutokea majira ya saa saba unusu usiku wa kuamkia leo Agosti 28, 2024.
Mkuu wa kitengo cha uhusiano mwema katika TRC, Jamila Mbarouk alielezea pia kwenye taarifa hiyo kwamba mabewa 6 yaliacha njia ya treni na kusababisha ajali hiyo.
Majeruhi wa kike ni 26 na wa kiume 44 na treni hiyo ilikuwa na jumla ya abiria 571 waliokuwa wakisafiri kutoka Kigoma kuelekea mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
TRC kwa ushirikiano na Kitengo cha afya cha mkoa wa Kigoma walifanikiwa kuwapeleka majeruhi katika Hospitali ya wilaya ya Uvinza kwa matibabu na inaripotiwa kwamba hali zao zinazidi kuimarika.
Majeruhi 57 walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka, wanane wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo ya wilaya ya Uvinza huku watano wakihamishiwa hospitali ya Maweni.
Treni hiyo baadaye iliendelea na safari kuelekea mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
TRC ilitoa pole kwa majeruhi na inaendelea na jitihada za kuwahudumia.