Gavana Mwangaza aidhinisha bajeti ya shilingi bilioni 11.8

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza, ametia saini bajeti ya shilingi bilioni 11.8 ya mwaka 2024/2025, siku chache baada ya Mahakama Kuu kusimamisha kutimuliwa kwake.

Akizungumza afisini mwake leo Ijumaa baada ya kutia saini bajeti hiyo, Gavana huyo aliwalaumu wawakilishi wadi kwa kupunguza bajeti ya afisi yake, hususan ile ya mafuta ya petroli aliyodai ilipunguzwa kutoka shilingi milioni 10 hadi shilingi milioni 3.

Gavana huyo pia alisema kuna fedha za miradi mingine ya maendeleo ambazo zilihamishwa kwa miradi mingine na wawakilishi hao wa wadi.

Hata hivyo alisema ameazimia kutia saini bajeti hiyo ili kuepusha kucheleweshwa kutekelezwa kwa miradi hiyo na malumbano na bunge la kaunti hiyo.

Bunge la Seneti lilikuwa limedumisha hatua ya bunge la kaunti ya Meru ya kumtimua Gavana Mwangaza, lakini Mahakama Kuu ikafutilia mbali hatua hiyo, hadi kesi iliyowasilishwa na Gavana huyo itasikilizwa na kuamuliwa.

Share This Article