Washukiwa watano wametiwa mbaroni kuhusiana na utekaji na ubakaji wa msichana wa umri wa miaka 16 katika kaunti ya Kilifi.
Kulingana na maafisa wa idara ya upelelezi wa jinai, DCI, msichana huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nane alikamatwa na watu hao akielekea nyumbani kutoka shuleni katika eneo la Mitangoni.
Inaaminika kwamba hatua hiyo ilichochewa na haja ya kulipiza kisasi kwani walikuwa na shida na babake.
Mshukiwa mkuu kwa jina Karisa Kashindo wa umri wa miaka 42 na mlinzi wake Nderi Magure Mwatsuma almaarufu Ubwete wa umri wa miaka 63 wanaripotiwa kuwa na mvutano unaohusu ardhi na baba ya msichana huyo tangu mwezi uliopita.
Elijah Dadi Robert, mshukiwa mwingine katika kisa hicho ambaye ana umri wa miaka 21, ametambuliwa kama aliyepanga njama ya kumteka nyara msichana huyo ambapo alimfungia kwenye tingatinga ambayo kwa sasa haitumiki.
Alipohojiwa, mhasiriwa wa kisa hicho alielezea kwamba alibakwa na wanaume wengine wengi wa umri mdogo ambao pia wamekamatwa.
Maafisa wa DCI walitaja washukiwa wengine ambao ni Fostine Kalu Tinga wa miaka 19 na Kelvin Kiti Sanga na kufafanua kwamba ni wanafunzi wa kidato cha pili na tatu mtawalia.
Msichana aliyetendewa unyama huo aliokolewa na kurejeshwa kwa familia yake huku washukiwa wakisalia kwenye korokoro za polisi kusubiri uchunguzi ukamilike.