Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania Kassim Majaliwa ametoa agizo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, afisi ya Rais-TAMISEMI, afisi ya Waziri Mkuu zishirikiane na Wizara ya Fedha kubuni mpango wa kitaifa wa kuwezesha vijana wanaoacha kutumia dawa za kulevya kujikimu.
Majaliwa anasema kutekelezwa kwa agizo hilo kutawawezesha vijana hao kupata mitaji ya kushiriki shughuli za ujasiriamali ili kukuza kipato chao.
Alitoa agizo hilo jana Jumapili, Juni 30, 2024 alipohutubia wananchi wa Tanzania na wadau mbalimbali walioshiriki kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupambana na dawa za kulevya duniani katika viwanja vya Nyamagana, jijini Mwanza.
“Wako wengine wanaohitaji kilimo, Wizara ya Kilimo itoe utaratibu, wapo wanaohitaji ufundi, Wizara ya Elimu itoe utaratibu, lengo ni kuhakikisha vijana hawa wakitoka huko wanakuwa na shughuli ya kufanya ili kujikimu,” alisema Majaliwa.
Alimtaka pia kamishna Jenerali pamoja na timu yake ya mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya aendelee kutekeleza operesheni dhidi ya dawa za kulevya kwenye mabasi, ndege, bandarini, vituo vya reli, masoko, maeneo yenye watu wengi na kote nchini Tanzania ili kuhakikisha usalama.