Idara ya magereza imewaachilia huru wafungwa 23,000 wa makosa madogo madogo, kwenye marekebisho yanayoendelea ya kupunguza idadi ya wafungwa.
Katibu katika idara hiyo Salome Muhia, alisema idara hiyo inanuia kuangazia upya hukumu za wafungwa 5,000, ili kuafikia lengo lake la kuwaachilia wafungwa 35,000 kufikia mwishoni mwa mwaka 2023. Baadhi ya wafungwa 7,281 wa makosa madogo-madogo, waliachiliwa huru mwezi Machi mwaka huu.
Afisa huyo aliyekuwa kwenye ziara rasmi ya magereza yote Kaunti ya Kisumu siku ya Ijumaa, aliahidi kushirikiana na idara ya mahakama na wadau wengine, ili kupunguza idadi ya wafungwa walio gerezani kote humu nchini kwa sababu ya makosa madogo-madogo.
“Nawahimiza washirika wengine kusaidia katika mpango huu wa kupunguza idadi ya wafungwa, kuhakikisha wafungwa wanaishi maisha nadhifu kuambatana na sehemu ya 28 na 43 ya katiba ya Kenya,”alisema katibu huyo katika gereza la Kodiaga.
Aidha katibu huyo alisema serikali itatumia vituo 135 vya urekebishaji tabia kote nchini, huku ikijadiliana na idara ya mahakama kuwahumu walio na makosa madogo madogo kushiriki huduma ya kijamii.
Muhia alipongeza mafunzo ya kiufundi yanayotolewa kwa wafungwa katika magereza mbali mbali, yanayowasaidia kutangamana kwa urahisi katika jamii.
Wengine waliokuwepo ni pamoja na kamishna wa magereza nchini John Warioba, katibu wa urekebishaji tabia Mary Mbau na kamanda wa idara ya magereza eneo la Nyanza Patrick Nyaachi miongoni mwa wengine.