Mama wa Taifa Rachel Ruto jana Jumapili aliongoza maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mjini Mwatate, kaunti ya Taita Taveta ambapo alihimiza watoto kupata elimu.
Mkewe Rais alisema watoto wanafaa kutumia fursa inayotolewa na serikali na washirika wa kimaendeleo kupata elimu ambayo itawasaidia siku za usoni.
Kulingana naye, serikali imejizatiti kuboresha sekta ya elimu nchini kwa njia mbalimbali kama vile kuhakikisha uwepo wa miundombinu hitajika na kuajiri walimu zaidi.
Bi. Ruto alisema hatua kama hizo ni dhihirisho la kujitolea kwa serikali kuboresha sekta hiyo muhimu. Alisema hata ingawa kuna changamoto, serikali imechukua hatua za kuonyesha kujitolea kwake kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wote nchini.
Siku ya Mtoto wa Afrika imekuwa ikiadhimishwa tarehe 16 mwezi Juni kila mwaka tangu mwaka 1991 wakati ilianzishwa na Shirika la Umoja wa Afrika, OAU wakati huo.
Ni siku ya kutoa heshima kwa walioshiriki maasi ya Soweto Juni 16, 1976 wakati watoto wa shule wa asili ya Afrika waligoma kulalamikia ubovu wa elimu waliokuwa wakipokea wakitaka wafundishwe kwa lugha yao ya asili.